BREAKING
BannerFans.com

Jumanne, 31 Januari 2017

FAHAMU ATHARI ZA MFADHAIKO (DEPRESSION) NA SULUHISHO LAKE


Asalaam alaykum warhmatullah wabarakatul, Alhamdulillah naendelea vyema nanyi pia wapenzi wasomaji wa blog hii natumaini muwazima
Naam,nina imani kila mmoja wetu ameshapata kuwa na huzuni wakati fulani, ni kitu cha kawaida kinachotokea wakati umepotelewa na kitu, kutokana na mihangaiko ya maisha au kutokana na kudharauliwa. Huzuni ikizidi na ikienda kwa siku nyingi mfululizo (wiki mbili au zaidi) na ikiambatana na hali ya kujiona kuwa si wa thamani tena, kwamba ni mtu usiye na msaada wowote  basi hii inaweza kuwa ni zaidi ya huzuni na ikawa yenye athari katika afya ya mwanadamu na hapo utakuwa umepata tatizo la kiafya mfadhaiko, ugonjwa ambao kwa bahati nzuri una tiba.

MFADHAIKO(DEPRESSION)
Ni ugonjwa unasababisha mtu kuwa na huzuni kila wakati na kukosa hamu ya kufanya vitu au kutenda yale aliyopenda sana kufanya zamani. Mfadhaiko ni ugonjwa unaoathiri namna mtu anavyojisikia, anavyofikiri na tabia yake.

CHANZO CHA MFADHAIKO(DEPRESSION)

Chanzo halisi cha ugonjwa huu mpaka sasa bado hakijafahamika Wataalamu wanasema kuwa ni muunganiko wa sababu nyingi ikiwa ni pamoja na urithi, mazingira ya maisha, mambo ambayo mtu amekutana nayo katika maisha na sababu za kisaikolojia.
Mtu anaweza kukutana na jambo moja tu kubwa na baya katika maisha yake kama kufiwa na mtu wa karibu, mahusiano mabaya ya ndoa au kubakwa na akapata mfadhaiko.
Mtu mwenye mfadhaiko hupungukiwa na uwezo wake wa kutenda kazi kiasi kwamba yeye na walio karibu naye wote huathirika.

Ugonjwa huu huwapata zaidi watu wanaokunywa sana pombe au kutumia madawa ya kulevya. Watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, wenye magonjwa ya moyo, waliopatwa na kiharusi, wenye kansa, kisukari, ugonjwa wa Parkinson’s na baadhi ya magonjwa mengine huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na mfadhaiko.
 Mtu mwenye mfadhaiko pamoja na magonjwa hayo mengine huwa kwenye hali mabaya zaidi ya kiafya na hupata shida zaidi kuutibu ugonjwa huu.

Utafiti wa zamani ulisema kuwa watu wenye matatizo ya mfadhaiko waliathirika kutokana na kutengwa na jamii, lakini utafiti wa hivi karibuni umetoa majibu tofauti na kuonyesha kwamba mtu anatengwa na jamii kutokana na mfadhaiko alio nao.

Mfadhaiko ni ugonjwa ambao umefahamika toka zamani sana. Ndugu Hippocrates aliuita ugonjwa huu Melancholia.

Watu wengi mashuhuri wameumwa ugonjwa huu na wengine katika maisha yao yote.
Abraham Lincoln, raisi wa 16 wa Marekani na Winston Churchil wa Uingereza ni baadhi ya watu walioumwa ugonjwa huu katika maisha yao yote.

AINA ZA MFADHAIKO(DEPRESSION)
Tatizo hili la kuwa na mfadhaiko linakuja kwa namna nyingi. Hapa chini ni baadhi ya aina za mfadhaiko

MAJOR DEPRESSIVE DISORDER (MAJOR DEPRESSION)

Mgonjwa mwenye aina hii ya mfadhaiko anakuwa na mchaganyiko wa dalili nyingi za mfadhaiko ambazo zitamfanya ashindwe kulala, kusoma, kufanya kazi, kula na kufaidi vitu ambavyo awali vilikuwa vinamvutia sana.
Aina hii ya mfadhaiko humpotezea kabisa mgonjwa uwezo wa kushiriki kwenye shughuli za kazi vizuri na Watu wengine hupatwa na hali hii mara moja wakati wengine hurudiwa mara nyingi zaidi

 DYSTHYMIA DISORDER(DYSTHYMIA)

Mgonjwa wa aina hii ya mfadhaiko anaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda mrefu, pengine miaka kadhaa, lakini hana dalili ambazo ni kali sana kama za aina ya kwanza hapo juu.
 Mgonjwa hufanya kazi zake ingawa si kwa ufanisi mkubwa na huwa si mtu mwenye raha kamili
 Watu wengine hupatwa na hali hii mara moja tu katika maisha yao wakati wengine hurudiwa mara nyingi
Mgonjwa wa aina hii ya mfadhaiko huweza kupatwa na aina ya kwanza hapo juu mara moja au zaidi katika maisha yake.

PSYCHOTICS DEPRESSION

Endapo mfadhaiko utakuwa mkubwa na kuambatana na mtu kuwa na maluweluwe (hallucinations) na kuwa nje ya maisha halisi, mtu huyu anaweza kuwa na aina ya mfadhaiko unaoitwa Psychotic depression, ugonjwa ambao mara nyingine huitwa delusional depression.

POSTPARTUM DEPRESSION POSTNATALl DEPRESSION DEPRESSION)

Hii ni aina ya mfadhaiko ambayo Mara nyingi huwapata wanawake waliotoka kujifungua,
Kama mama mzazi atapatwa na mfadhaiko wiki chache baada ya kujifungua, anaweza kuwa amepatwa na postnatal depression.
 Wataalamu wanasema kuwa asilimia 15 hadi 20 ya akina mama hupatwa na ugonjwa huu baada ya kujifunga, bahati mbaya ni kwamba wengi hawagunduliki na wanateseka kwa miaka mingi baada ya kujifungua. Mama anaweza kuupata ugonjwa huu muda wowote katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kujifungua.

SAD (SEASONAL AFFECTIVE DISORDER)

Idadi ya watu wanaopatwa na ugonjwa huu huoongezeka zaidi kadiri unavyokwenda mbali zaidi na Ikweta.
 Mwisho wa kipindi cha summer ni mwanzo wa kuona jua kwa muda mfupi zaidi au mwanzo wa saa nyingi zaidi za giza kwa siku.
 Mtu anayepatwa na mfadhaiko katika kipindi hiki huweza kuwa amepata aina hii ya ugonjwa
Ugonjwa huu hutoweka wenyewe wakati wa spring au summer.

BIPOLAR DISORDER (MANIAS  DEPRESSIVE  ILLNESS)

Aina hii ya mfadhaiko haionekani kwa wingi kama aina nyingine za hapo juu. Tabia kuu ya aina hii ya mfadhaiko ni kuwa na vipindi vya dalili kuwa juu sana na baadaye kushuka. Viwango hivi vya juu na chini huitwa manias.

DALILI ZA MFADHAIKO(DEPRESSION)

Zifuatazo ni dalili za mfadhaiko

(1)kutopenda kushirikiana na watu wengine
(2)Kuwa na huzuni kila wakati na kujiona kuwa ni mtu usiyefaa
(3)Kukosa mwamko na hamu ya kufanya shughuli/Matatizo katika kufanya maamuzi
(4)Kutotulia na kuwa na hasira
(5)Kula zaidi au pungufu ya kawaida
(6)Kulala zaidi au pungufu ya kawaida
(7)Kushindwa kutuliza mawazo kwenye jambo
(8)Matatizo ya kumbukumbu
(8)kukosa raha ya maisha
(9)Kukosa hamu ya kuanya mambo uliyoyapenda sana zamani na         hamu ya kufanya mapenzi
(10)Kujisika vibaya juu yako au kuwa mwenye makosa
(1)Kuona kwamba huwezi kutatua matatizo yako ya maisha
(12(Kuumwa kichwa kubanwa misuli, matatizo ya uyeyushaji chakula tumboni, matatizo ambayo hayaponi kwa kutumia dawa
(13)Kuwa na mawazo ya kujiua

NAMNA YA KUONDOA MFADHAIKO
Mfadhaiko ni kitu ambacho kinakupunguzia nguvu zako za kufanya kazi, kinachokukatisha tamaa na hivyo kuzuia jitihada zako za kutaka kupambana na matatizo uliyo nayo.
Unaweza kuondokana na tatizo hili kwa kuwaona wataalamu wa magonjwa ya akili, kwa kutumia dawa au kupambana nalo mwenyewe. Mada ya leo ni kuhusu namna ya kuondoa mfadhaiko wewe mwenywe kwa kutumia njia ambazo hazihitaji dawa au mtaalamu; kwa kubadili staili ya maisha yako, kubadili tabia yako na kubadili namna yako ya kufikiri.

Pamoja na kuwa ni kazi kubwa kuondoa tatizo la mfadhaiko ulilo nalo, haimaanishi kwamba ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa – inawezekana, kwa kuanza taratibu na kuongeza jitihada kila siku, hata kama mfadhaiko wako ni mkubwa kiasi gani. Kupambana na mfadhaiko ni kazi inayohitaji uamuzi na kuanza kutenda wakati ambapo haupo ndani ya hali yako ya mfadhaiko. Vitu ambavyo utahitaji kuvifanya ili vikusaidie ndivyo vitu vigumu lakini ugumu wa vitu hivyo haumaanishi kwamba hutoweza kuvifanya. Itachukuwa muda kufikia kwenye hali yako nzuri ya kawaida lakini msimamo thabiti wa kutaka kukabiliana na tatizo hili utakusaidia kufanikiwa.

Utahitaji kujiwekea malengo machache na rahisi ya kuanza nayo na taratibu kujijenga kuanzia hapo. Tumia njia zote unazoweza kupata, anza na vitu vichache na kila siku hakikisha unafanya kitu fulani. Pima maendeleo yako na usikose kujipongeza pale unapopiga hatua. Hatua tutakazokupa hapa unaweza kuona kama ni ndogo na ukazibeza lakini haraka zinajijumuisha na kukupa matokeo mazuri katika kupambana na tatizo lako. Anza kwa kufanya yafuatayo:

1. JENGA MAHUSIANO YA KUSAIDIANA

Kupata msaada ni jambo ambalo litakusaidia sana katika kuondoa wingu la mfadhaiko lililoko mbele yako, peke yako itakuwa vigumu kuendelea na jitihada zako za kupambana na tataizo hili. Mfadhaiko kwa tabia yake, utakuzuia kutoka na kwenda kuomba msaada kwa watu wengine, lakini elewa kuwa kujitenga na upweke vinachangia kuukuza mfadhaiko ulio nao.

Utajisikia kuwa ni jambo gumu sana kwako kwenda kukutana na ndugu wa karibu na marafiki zako. Utaona kwako kuwa hilo ni jambo la aibu, litakalokuchosha, au kujisikia mkosefu kwa kuyavunja mahusiano ya awali, kwa taarifa yako, huu ndiyo mfadhaiko ulio nao ukifanya kazi yake. Kuwafuata jamaa zako si kuonyesha udhaifu na wala sio kuwa kero kwa wenzako. Watu wa karibu yako wanakujali na wapo tayari kusaidiana na wewe. Anza sasa, hujachelewa kamwe.

Washirikishe jamaa wa karibu: Eleza tatizo lako kwa watu unaowaamini, wafuate na zungumza nao ana kwa ana. Omba msaada wao, watakuwa tayari kukusaidia pamoja na kwamba ulijitoa nje ya mahusianao nao.

Jichanganye kwenye shughuli: Mara nyingi utakapokuwa kwenye mfadhaiko utapenda kujitenga na kubaki peke yako, hali ikizidi kubaki palepale tofauti na pale utakapochinganya kwenye shughuli za kijamii ambapo mfadhaiko wako utapungua. Jitahidi kujichanganya hata kama hufurahishwi sana na shughuli hizo. Jaribu haya machache kwa kuanza kujenga mahusiano na watu:

Zungumza na mtu mmoja kuhusu matatizo yako
Msaidie mtu mwenye matatizo
Pata chakula cha mchana au kahawa na rafiki
Kutana na umpendaye mara kwa mara
Msindikie mtu kuona tamasha au kongamano
Mpigie simu rafiki
Panga ratiba ya kupata chakula cha jioni na marafiki
Kutana na watu kwa kujiunga na masomo au michezo
Fanya matembezi
Mwone mtaalamu wa tiba ya akili au mtu wa ushauri

 2. PAMBANA NA MAWAZO HASI

Mfadhaiko hukufanya ukione kila kitu kuwa ni kibaya, wewe mwenyewe, mazingira unamoishi na mategemeo yako ya baadaye. Suluhu hapa ni kuyaondoa haya mawazo mabaya na kupandikiza badala yake mawazo mazuri.

Namna ya kuondoa mawazo hasi

Acha kiudhuru nafsi yako: Kuna mambo mengi ambayo huwa unayafikiria sana kuhusu nafsi yako. Jee, hayo mambo unayoyafikiria ni mambo ambayo ungethubutu kumsimulia mtu mwingine? Kama jibu ni hapana, acha kuihujumu nafsi yako na anza kufikiria mambo ambayo si mazito sana kuhusu nafsi yako.

Usijione kuwa wewe ndiye mkamilifu: Watu wengi wanaopata mfadhaiko ni wale ambao hujiona kuwa wao ni wakamilifu, hujiwekea viwango vikubwa sana vya maisha na pale inapotokea kuwa wanashindwa kuvifikia viwango hivyo wanaanza kujiona kuwa ni watu wasiofaa. Epuka kujipa mfadhaiko mwenyewe kwa kuacha kuwa na mawazo potofu.

Jichanganye na watu wenye mawazo mazuri: Hebu jaribu kuwatazama watu wenye mtazamo mzuri kuhusu maisha wanavyopambana na vikwazo vya maisha hata kwenye kitu kidogo tu kama vile kufika eneo fulani na kukosa sehemu ya kupaki gari. Wewe ungefanyaje hapo? Jaribu kuiga wanavyofanya hawa watu, hata kama ni kwa kujifanya tu (haitoki rohoni) na endelea kufanya hivyo hivyo, kiuchangamfu, kwenye mazingira mengine ya vikwazo.

Orodhesha mawazo mabaya yanayokujia: Kila wakati ukijiwa na wazo baya, liandike na nini kilisababisha upate wazo hilo. Wakati ambapo kichwa chako kimetulia, pitia mawazo haya na yajadili kama ni kweli yalifaa kuwaziwa. Litazame wazo lako kwa mtazamo mwingine tofauti; mpenzi wako kakuudhi, ukaamua kuwa huo ulikuwa mwisho wa mahusiano yenu, jee haiwezekani, kwa mfano, kuwa mwenzio alikuwa kwenye wakati wake mbaya?



3. LEA MWILI WAKO VYEMA

Ili kuudhibiti mfadhaiko ni lazima uulee mwili wako, ikimaanisha kuwa na mtindo wa maisha unaofaa, kujua namna ya kuudhiti mafadhaiko, kujua viwango vinavyoweza kufikiwa na mwili wako na kuweka kwenye ratiba muda wa kuuburudisha mwili wako.

Hakikisha unapata usingizi wa kutosha: Mfadhaiko kwa kawaida huendana na matatizo ya usingizi, unaweza kulala kupita kiasi au ukakosa usingizi. Vyote ni vibaya kwako. Tafata njia za kupata usingizi kwa muda wa saa 8 kwa siku.

Pata muda wa kukaa nje kila siku:Kukosa mwanga wa jua kunaweza kuifanya hali yako ya kuwa na mfadhaiko kuongezeka. Fanya matembezi nje, pata kahawa yako nje, kaa katika bustani n.k. Lenga kupata angalau dakika 15 za kukaa juani kila siku.
Kuwa makini na msongo wa mawazo:Msongo wa mawazo unaongeza muda wa kuwa na mfadhaiko, unaongeza ukubwa wa mfadhaiko na kusababisha mfadhaiko. Vichunguze vitu vyote vinavyokusababishia msongo wa mawazo, kazi nyingi, mahusiano ya kijamii, matatizo ya kiafya n.k. kisha weka mipango ya kukwepa vyanzo hivyo
Mazoezi ya kupumzisha mwili: Kuwa na ratiba ya kila siku ya mazoezi ya kupumzisha mwili kunaweza kuondoa mfadhaiko. Jaribu vitu kama yoga, meditation, deep breething n.k.

4. FANYA MAZOEZI KILA WAKATI

Unapokuwa na mfadhaiko, mazoezi ni kitu cha mwisho ambacho mwili utapenda kufanya, lakini mazoezi ni kitu chenye nguvu sana katika kuondoa mfadhaiko. Utafiti umeonyesha kuwa mazoezi yana nguvu sawa na dawa za kuondoa mawazo. Sababu kamili haijaeleweka, lakini fikra moja ni kwamba mazoezi yanawezesha uzalishaji wa seli mpya katika ubongo

Jiwekee ratiba ya mazoezi ya nusu saa kila siku ukianza na mazoezi laini au mazoezi mazito kidogo kwa dakika kumi. Unaweza kufanya yafuatayo:

Panda ngazi badala ya kutumia lifti
Paki gari yako kwenye sehemu iliyo mbali kuliko zote
Tafuta rafiki wa kufanya naye mazoezi
Tembea wakati unazungumza na simu

 5. KULA CHAKULA BORA
Chakula unachokula kina uhusiano na namna utakavyojisikia kimwili. Hakikisha unapata mlo kamili wenye protini isiyo na mafuta sana, chakula chenye wanga, matunda na mboga. Punguza matumizi ya kahawa, pombe na chakula kilichosindikwa kwa kemikali.

Usiruke milo: Kukaa muda mrefu bila kupata kitu cho chote kunaweza kukufanya ukose raha na kuwa mchovu, jaribu kula kitu fulani kila baada ya saa 3 au 4.

Punguza sukari na chakula kilichokobolewa: Chakula chenye sukari kwa wingi, kama vile vitu vidogo vidogo vya kutafuna (snacks) na pasta, vinaburudisha kwa muda mfupi lakini baadaye vinakusababishia kuingia kwenye hali ya fikra na kukupunguzia nguvu za mwili.

Tumia vitamini B: Upungufu wa vitamini B kama folic acid au B12 unaweza kusababisha mfadhaiko. Tumia vidonge vya vitamini B-complex au ipate vitamini hiyo kutoka kwenye matunda, mboga za majani, maharage, nyama ya kuku na mayai.
Tumia chakula chenye viini-lishe kwa wingi kama ndizi (magnesium kupunguza wasiwasi, vitamini B6 kukupa umakini, tryptophan kuongeza kiwango cha serotonin), spinach (magnesium, folate kupunguza hali ya kuhangaika na kukupa usingizi) na brown rice (serotonin, thiamine).

Omega-3 fatty acids: Chakula chenye Omega-3 fatty acids hukufanya ujisike vizuri. Chanzo cha Omega-3 fatty acids ni samaki wenye mafuta (salmon, sardines n.k.).

6. TAFUTA MSAADA WA KUONDOA MFADHAIKO

Kama mfadhaiko wako unazidi kuwa mbaya, omba msaada kutoka kwa wataalamu, kufanya hivyo si dalili ya udhaifu. Mawazo chanya unayoyapata kutokana na mfadhaiko wako yanaweza kukufanya ukajioona kuwa wewe sasa ndio umefika mwisho, kwamba huna ujanja tena wa kujinasua. Kumbuka kuwa mfadhaiko ni ugonjwa tu, na unatibika. Zingatia dondoo za hapo juu kuhusu kujisaidia kupambana na mfadhaiko hata kama utapata ushauri wa kitaalamu kwani zitakusaidia uondokane na mfadahiko mapema zaidi na kusaidia ugonjwa huu usirudie tena.

Mpendwa msomaji nashukuru Kwa kuchukua muda wako kufatilia makala zangu za afya nasema ASANTE NA MUNGU AKULIPE KHERY PIA IKIWA UNA MAONI AU USHAURI NIANDIKIE UJUMBE  KUPITIA KATIKA EMAIL AU NAMBA ZANGU HAPO CHINI

KUSOMA ZAIDI MAKALA MBALIMBALI  ZA AFYA TEMBELEA
 NAYTHAMHEALTHCARE.BLOGSPOT.COM

 ~Makala hii imeandaliwa na Dr Naytham Salum
E-mail nsalum998@gmail.com
+255623026602/+255746465095

Hakuna maoni :